Wanachama 6 wa FRONADER Ingabo z' Umwami wapandishwa kizimbani
Wanajeshi 6 wanaojitambulisha kama wanachama wa FRONADER Ingabo z’ Umwami, yaani FRONADER Majeshi ya Mfalme kwa kiswahili, ijumaa iliyopita walifikishwa kwenye mahakama kuu ya Nyarugenge.
Washukiwa sita wanaokiri kuwa wanachama wa
FRONADER Ingabo z' Umwami
Wanajeshi hao wote 6 wanakabiliwa na tuhuma za kuhatarisha usalama wa taifa, kuunda kundi la kigaidi, na kuratibu njama za kutimua madarakani serikali iliyopo nchini Rwanda.
Washukiwa wote sita wakiwemo hata aliyekuwa askari katika majeshi ya EX-FAR maarufu kwa jina la kanali Gaheza, walikubali kuhusiana na tuhuma zote dhidi yao na kuomba msamaha.
Huku wengi wao wakisema kuwa walikipa uungaji mkono chama cha FRONADER Ingabo z’ Umwami bila kujua mipango yake halisi, mmoja tu kati yao ndiye alikiri kuwa alijiunga na chama hicho kwa vile anavyompenda mfalme Kigali Ndahingurwa ambaye kwa sasa anaishi marekani ambapo alienda baada ya ufalme wake kupinduliwa.
Chama cha FRONADER Ingabo z’ Umwami kinadaiwa kuwa na makao yake nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na kinadaiwa kuwa na fungamano kubwa na chama kingine cha upinzani kijulikanacho kama CNR Intwari ambacho mwenyekiti wake ni aliyewahi kuwa waziri wa jeshi hapa Rwanda, Emmanuel Habyarimana.
Vilevile washtakiwa hao walikiri kuwa na uungaji mkono wa chama kinachotawaliwa na Kayumba Nyamwasa, ambaye pia alikuwa amri jeshi hadi mwaka 2003 kabla ya kuteuliwa kuwa balozi wa Rwanda nchini India hadi februari 2011 alipoamua kuikimbia serikali ya Rwanda na kuhamia nchini Afrika ya Kusini.
Inatarajiwa kuwa jumatatu tarehe 11 julai ndipo mahakama itatangaza uamuzi wake kuhusu iwapo washukiwa watapewa dhamana au la.
Kuhusiana na hilo, uendeshaji wa mashtaka uliomba mahakama kuwakatalia dhamana washukiwa kwa kuwa kufunguliwa kwao kunaweza kuathiri vibaya juhudi za upelelezi.